Alhamisi, 23 Oktoba 2014

ZAWADI MUHIMU KWA MTOTO


Tumezoea kuwanunulia watoto wetu zawadi mbalimbali hasa katika siku muhimu kama kumbukumbu ya kuzaliwa. Mara nyingi zawadi hizo wanazifurahia sana wanapozipata na baada ya muda mfupi wanapoteza hamu nazo. Kuna zawadi za muhimu sana kwa mtoto wako na atakuwa nazo mwaka mzima na kuzifurahia siku zote.

1.Zawadi  ya Upendo
Muonyeshe mtoto wako kuwa unampenda kwa maneno na vitendo. Mkumbatie mara kwa mara hasa wakati akiwa na huzuni au hofu na umwambie ni jinsi gani unampenda na unashukuru Mungu kuwa naye kama mtoto wako.

2. Zawadi ya Maonyo
Unapoacha kumuonya mtoto pale anapokosea unakuwa unachangia katika kuyaharibu maisha yake. Mfundishe mtoto utii kwa wazazi na watu wote na hivyo atakuwa anamtii Mungu, na usiache kumuonya pale anapokosea.

3. Zawadi ya Muda
Uwe na muda wa kufurahi na kucheka na mtoto wako. Upatikane kwake pale anapokuhitaji akusimulie hadithi zake, akuulize maswali au tu kupata muda wa kuwa nawewe. Umpe muda wako bila masharti yoyote na awe huru kuwa na wewe bila kujisikia vibaya.

4. Zawadi ya Ukarimu
Mtoto anapofikia umri wa kuanza shule na kujenga marafiki kuna wakati atakuwa anakuja nao nyumbani. Mwonyeshe zawadi ya ukarimu kwa kuwakarimu marafiki zake na kutaka kuwafahamu zaidi.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni