Alhamisi, 2 Oktoba 2014

WAJIBU WA MZAZI KWA MTOTO WAKE




Tunazungumza kuhusu wajibu wa mzazi kwa watoto katika malezi bora na yenye kuleta manufaa kwa Taifa ambalo ni  jamii inayotuzunguka pamoja na Mungu, kubadili tabia na kujua wajibu wako kama mzazi bora.

Wajibu wa mzazi kumpatia mtoto mapumziko unapaswa kupewa msukomo wa kipekee. Ni wajibu ambao unachangia kukua kwa mtoto katika nyanja za kiutamaduni, kisaikolojia, uhusiano na ubunifu. Mtoto anapopata nafasi ya kucheza, kupumzika na kujifunza kuhusu mazingira yake na hasa masuala ya kiutamaduni hujifunza mengi ambayo hawezi kujifunza kwa namna nyingine.

Mtoto anapopata fursa hii ndipo anapoweza kubaini namna ya kutatua matatizo mbalimbali ya kibinafsi na kijamii. Wajibu huu ni jukumu la wazazi lenye lengo la kumjenga mtoto kiakili, kijamii, kimaadili, kiutamaduni na kisaikolojia. Hapo ndipo wajibu huu unapokuwa ni haki ya msingi ya mtoto.

Wajibu wa kumpatia mtoto elimu, afya, malazi na chakula unatokana na nafasi yetu kibinadamu, kijamii na kisheria. Wajibu huu hautegemei tu mapenzi ya mzazi kwa mtoto wake, bali uwepo wa miundombinu, mitazamo ya kijamii na uwezo wa kifedha au kiuchumi wa mzazi.

Wajibu huu ni vyema umebainishwa kisheria ili jamii ielewe kwamba siyo chaguo la mzazi, bali ni la msingi kabisa. Serikali ina jukumu kubwa la kuhakikisha siyo tu inasimamia utekelezaji wa wajibu huu, bali pia kuwawezesha wazazi na jamii ambayo haina uwezo wa kutekeleza wajibu huu.


Ukweli ni kwamba, pamoja na sheria kuwepo, watoto wenye wazazi walio na kipato kidogo au wasio na kipato kabisa, hawataweza kufaidi upatikanaji mzuri wa huduma hizi. Utekelezaji wa wajibu huu ni lazima uambatane na msukumo wa serikali wa kutimiza wajibu wake kwanza na kuondoa vikwazo vyote, viwe vya kimiundombinu, kiutendaji au kiuchumi.Wazazi wengi wanaweza kupuuza wajibu wao wa kumpatia mtoto heshima na utu.

Mtoto anaweza kupoteza uwezo wa kujithamini na kujiamini mbele ya jamii na hivyo kumsukuma katika matatizo mengine, ya kisaikolojia, kiakili na kiroho tangu umri wa utoto mpaka utu uzima. Matizo haya huleta athari kwa mtoto, familia na nchi kwa ujumla katika nyanja zote.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni