Kwa miezi sita ya
kwanza katika maisha ya mtoto chakula pekee ambacho wataalamu wa afya
wanashauri apewe ni maziwa ya mama tu. Kunyonyesha ndio njia ya kwanza kabisa
kumpa mtoto chakula. Unapoanza kumpa mtoto vitu vingine kama maziwa ya kopo
wakati ana miezi michache utoaji wako wa maziwa unaathirika maana jinsi mtoto
anavyonyonya ndivyo jinsi maziwa yanavyotengenezwa ndio maana watu wengi
wanavyoanza kazi na kumuacha mtoto nyumbani maziwa yao yanaanza kupungua.
Faida za kunyonyesha maziwa ya mama ni pamoja
na:
Maziwa ya mama yana
virutubisho vingi vya asili ambavyo ni muhimu sana katika ukuaji na kinga kwa
mtoto. Humlinda na magonjwa mengi ya utoto pamoja na ‘allergies’ mbalimbali.
·
Hukuwezesha kuwa na ukaribu na mtoto wako.
·
Hukupunguzia uwezekano wa kupata kansa ya matiti.
·
Ni bure na unaweza kumpatia maziwa wakati wowote bila usumbufu.
Wakati
gani Uanze Vyakula Vingine
Mtoto wako akifikisha
miezi 6 unaweza kuanza kumpatia vyakula vingine kidogo kidogo (Kuna ambao kutokana
na sababu Fulani daktari huwashauri kuanza mtoto akiwa na miezi 4 hivyo ni vyema ukiwasiliana na daktari wako kwanza).
Mtoto akianza kupewa vyakula nje ya maziwa mapema kabla ya miezi 4 ni hatari
kwa afya yake maana mfumo wake wa kusaga chakula unakuwa bado haujawa tayari.
Unapoanza kumpa vyakula vingine hauachi kumnyonyesha, unyonyeshaji unaendelea
hadi miaka miwili na nusu.
Dalili
kuwa mtoto wako yupo tayari kuanza vyakula vingine ni:
·
Amefikisha miezi 6
·
Anaweza kushikilia kichwa juu ( shingo imekaza)
·
Anaweza kukaa kwa kuwekewa kitu ( mfano kiti chenye mkanda)
·
Unapompa chakula na kijiko anafungua mdomo kutaka kupokea au anageuza uso kwa
kukataa
·
Akipokea chakula anakiweka mdomoni na kujaribu kumeza na sio kukisukuma nje na
kuacha mdomo wazi.
Miezi
6-9
Endelea kunyonyesha na
anza kumpa vyakula vyenye madini ya chuma. Mtoto alishwe kwa ratiba
inayoeleweka kila siku na katika ratiba hiyo hakikisha angalau mara moja kwa
siku muda wake wa kula unakuwa sawa na muda wa familia yote ili muweze kula
pamoja. Vyakula vyake viwe vimepondwapondwa kabisa ikiwezekana tumia blender na
hakikisha anapata mlo kamili yani matunda, mbogamboga, mbegu, nafaka, nyama na
samaki. Inashauriwa kutokuchanganya aina tofauti za nafaka kwenye unga mmoja
unapomtengenezea uji, uwe na unga wa mahindi, ulezi,mchele n.k tofauti tofauti.
Pika aina moja ya uji kwa wakati unaweza kufanya kwa wiki au vyovyote utakavyopenda.
Unapompa mboga au
matunda anza na tunda moja moja kwa wakati. Osha vizuri matunda yako na
katakata vizuri na kuponda ponda kisha mpe kiasi kidogo kwa wakati na kikibaki
usikiweke, mtengenezee kile atakachokula tu. Matunda kama papai, parachichi na
embe ni mazuri kwa kuanzia. Chemsha maharage, njegere au mboga za majani na
kumpa supu kidogo kidogo, usiweke chumvi nyingi kidogo sana inatosha. Usimpe
juisi za madukani, hakikisha unamtengenezea juisi wewe mwenyewe na usichanganye
matunda mbalimbali kwenye juisi moja, na usiweke sukari kabisa.
Miezi
9-12
Katika umri huu mtoto
anakuwa tayari amezoea ladha tofauti tofauti za vyakula mbalimbali nje ya
maziwa. Anauwezo wa kukaa na kushikilia kitu kwa mikono yake na kuweka mdomoni hivyo
anza kumpa matunda laini mkononi aanze kujifunza kula mwenyewe. Hakikisha
vipande sio vidogo sana anavyoweza kumeza ili kuepuka hatari ya kukabwa. Kwa
sababu pia atakuwa ameanza kuota meno atakuwa anapenda sana kutafuna tafuna.
Katika umri huu pia unaweza kuanza kumpa kiini cha yai, ute wa yai hadi afike
umri wa mwaka mmoja. Endelea kumnyonyesha ila kwa sasa anakula kwanza kisha
ndio ananyonya maana akinyonya sana anaweza akakataa chakula. Usimpe chakula
kimoja mfululizo kwa muda mrefu maana atakinai na kuanza kukataa chakula, mpe
vyakula tofauti tofauti ili aendelee kupenda chakula.
Usalama
katika Kula
·
Hakikisha haumuachi mtoto mdogo na chakula au kinywaji bila uangalizi hata kama
ni maziwa ya chupa asije akapaliwa. Usimpe mtoto chakula au maziwa akiwa
amelala, analia au anacheka.
·
Usimpe chakula ambacho kinaweza kumkaba au kumpalia kama karanga, maindi,
zabibu n.k
·
Kabla ya kumpa mtoto chakula hakikisha umekiangalia joto lake usije ukamuunguza
mdomo.
·
Usafi wa mtayarishaji, mlishaji na mlishwaji ni muhimu san asana.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni