Watafiti wa masuala ya
haki za binadamu wamefanya utafiti na kutoa taarifa kwamba wapo watoto
magerezani wanaochanganywa na watu wazima, hivyo kuainisha kuwa hayo ni mateso
makubwa kwa watoto kisaikolojia na kimakuzi.
Sheria
zinaruhusu watoto watukutu kuwekwa kifungoni, ila si kwa lengo la kuwapa
adhabu, bali kuwapa mafunzo, lakini inapofikia hatua ya kuwekwa na watu wazima
ambao wengi wao huwa wana makosa makubwa na tabia za ajabu, si jambo zuri kwa
watoto.
Watoto wote wanahitaji
ulinzi, kufundishwa maadili na kupewa makuzi mazuri yasiyo na misukosuko kama
ile ya gerezani, kwani hata jela za watoto programu zake ni tofauti na zile za
watu wazima.
Wakati wafungwa watu
wazima wanapofanyishwa kazi kama vile za mashambani, ujenzi wa barabara,
uchimbaji mawe na nyinginezo ngumu, watoto wanapaswa wapewe kazi ndogondogo
kama vile za usafi na baadaye wawekewe walimu kwa ajili ya kuwapa elimu kwa
mujibu wa viwango vyao vya ufahamu, ili hata wakitoka jela, wasiwe wameachwa
mbali na wenzao waliokuwa shuleni.
Watoto wakiwa kifungoni
na wakipewa mafunzo mema, wengi wao hubadilika kwa sababu tayari wameonyeshwa
mwanga na pengine ni mazingira ndiyo yaliyosababisha wao kuwa watukutu, hivyo
jamii inapaswa kuwapa mazingira mengine mazuri ya kujifunza na wala si ya
kuwaumiza kisaikolojia na hata kuwapa madhara ya kimaumbile.
Uwepo utaratibu wa
kuwatenga watoto na watu wazima katika maeneo kama ya jela, ambayo kimsingi
kwanza mtoto si pahali pake, kwake yeye ni nyumbani ambako tunatarajia kuwa
ndiko atakakopatiwa malezi, ikiwa itabidi awekwe mbali na wazazi/walezi wake,
basi awekwe katika mazingira rafiki kwa afya yake ya kiakili na kimwili.
Yameibuliwa mengi, na
mengine ya kutisha bila shaka hayakutajwa katika utafiti, sisi tunaungana na
Tume ya Haki za Binadamu kuishauri serikali kuweka sehemu tofauti kwa kinamama
wenye watoto wadogo ikiwa mama hao watakutwa na kadhia zitakazowalazimisha
wawekwe kifungoni au kizuizini.
Jambo hilo kwa kawaida
halihitaji hata kutungiwa sheria, bali dhamira tu ya kibinadamu inabidi itusute
na kuona kuwa watoto hawastahili kuishi katika mazingira hatarishi. Mambo kama
haya kwa kweli si ya kuyafumbia macho, na tunatarajia kuwa serikali yetu sikivu
itakuwa imeyasikia na kudhamiria kuyafanyia kazi kwani ni wazi kuwa watoto hawa
watakapomaliza kifungo chao, kuja kuwa raia wema katika jamii itakuwa ngumu
kama ngamia kupita katika tundu ya sindano.
Tulidhani hili Serikali
inaliona na haikupaswa isubiri iumbuliwe na utafiti, wakati sasa umefika wa
kutoa kipaumbele katika ujenzi wa jela za watoto na sehemu za kuwaweka wanawake
wenye watoto wanapokumbwa na mkono wa sheria.
Sababu za kuwa Serikali
haina fedha, si sababu za kuridhisha, kwani vipo vipaumbele vingine vya
Serikali ambavyo hupatiwa fedha kwa udi na ubani, hivyo hili la watoto nalo la
kuwapatia mazingira salama, inabidi tuliweke katika vipaumbele vyetu
vinavyochukua nafasi ya kwanza.
Tume ya Haki za
Binadamu imefanya kazi yake ya kuibua madhila ya ukandamizaji wa haki za watoto
katika jamii, sasa kazi iliyosalia ni ya serikali na jamii kwa upana wake,
wakati umefika wa kulivalia njuga suala hili, kwa pamoja tupinge unyanyasaji
huu mkubwa kwa watoto kwani ni aibu kwa taifa.